KCSE Revision AI kcserevision.app

KCSE 2025 Kiswahili Paper 3

The KCSE 2025 Kiswahili Paper 3 (102/3). Fasihi: riwaya, tamthilia, hadithi fupi, ushairi na fasihi simulizi. View it below, download it to print, or revise it with the AI tutor, which takes you through each question and marks your answers. Source: KNEC.

102/3 · KISWAHILI · Karatasi ya 3 (Fasihi) · Nov. 2025 · Saa 2½

Maagizo: Jibu maswali manne pekee. Swali la kwanza ni la lazima. Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki, yaani Riwaya, Hadithi Fupi, Ushairi na Fasihi Simulizi. Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.

Sehemu A: Tamthilia — T. M. Arege: Bembea ya Maisha

1. (Lazima)
(a) "Maisha ni kujaribu. Kwa akina sisi mahuluku taabu, sawa na mtu aliyetapatapa kwenye mafuriko, lazima kushikilia chochote na popote mradi upate kusalimika."
(i) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
(ii) Bainisha aina mbili za taswira katika dondoo hili. (alama 2)
(iii) Fafanua umuhimu wa mzungumzaji katika kujenga tamthilia ya Bembea ya Maisha. (alama 8)
(b) Eleza jinsi mbinu rejeshi ilivyotumiwa kukuza maudhui katika tamthilia ya Bembea ya Maisha. (alama 6)

Sehemu B: Riwaya — C. Momanyi: Nguu za Jadi

Jibu swali la 2 au la 3.

2. "Lililo muhimu kwake ni mchango mdogo atakaoweza kutoa ili kubadilisha fikra za watu wake. Fikra zilienda mrama kwani baadhi yao hawakujua kilichowafurusha. Alitaka kulipigia mbizi tatizo lililowakabili."
(a) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
(b) Bainisha toni katika dondoo hili. (alama 2)
(c) Fafanua umuhimu wa mbinu mbili za kimtindo zilizotumiwa katika dondoo hili. (alama 4)
(d) Jadili umuhimu wa mhusika anayerejelewa katika dondoo hili. (alama 10)

3. (a) Changanua mtindo katika dondoo lifuatalo: (alama 6)
"Balaa gani hii sasa? Alitazamia kujenga duka la jumla na kufungua ukurasa mpya katika maisha yake. Ukurasa ambao kila mtu angetaka kuwa nao. Ukurasa wa heri na buraha. Wakati watu wanasaka kazi zisizopatikana na kukimbiza hela zilizowakimbia, yeye angestaladhi tu."
(b) "Mtemi Lesulia alitegemea jasho la raia kujinufaisha pamoja na mabarakala wenzake." Thibitisha kauli hii kwa kurejelea riwaya ya Nguu za Jadi. (alama 14)

Sehemu C: Hadithi Fupi — D. W. Lutomia na P. Muthama (Wah.): Mapambazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Jibu swali la 4 au la 5.

4. R. Timammy: "Ahadi ni Deni"
(a) "… alikuwa hata hampi nafasi ya kusema lolote. Alikuwa anafoka na alijua hata akijaribu kumweleza ingekuwa ni kazi bure. Asojua maana haambiwi maana."
(i) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
(ii) Bainisha umuhimu wa vipengele vifuatavyo vya kimtindo katika dondoo hili: (I) uradidi (II) taswira (alama 4)
(iii) Fafanua umuhimu wa mhusika anayerejelewa katika dondoo hili katika kujenga hadithi ya "Ahadi ni Deni." (alama 6)
(b) Jadili umuhimu wa matumizi ya barua katika kujenga hadithi ya "Kifo cha Suluhu." (alama 6)

5. Eleza jinsi mandhari yalivyotumiwa kukuza vipengele vifuatavyo katika hadithi ya "Nilitamani": (a) maudhui (alama 10) (b) wahusika (alama 10)

Sehemu D: Ushairi

Jibu swali la 6 au la 7.

6. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

Ukiwa naye rafiki ....
Wa kujifanya ni rafiki, jua likiwapo angani,
Giza linapotamalaki maningani haonekani,
Hivi wasema una nini?
Siyo rafiki, una popo!

Ukiwa naye rafiki ....
Wewe anayekuthamini, wakati awapo shidani,
Anayekuzonga rohoni, akitumani umuauni,
Kisha akiwapo rahani, anakuondoka machoni,
Hivi wasema una nini?
Siyo rafiki ni kunguni!

Ukiwa naye rafiki ....
Anayekujia nyumbani, akikuita 'we mwandani,
U rafiki aso kifani, tena mwenye mwingi uzani,
Amekufutika lindini, umezama kwake moyoni,
Na kisha awapo gizani, anakusema wewe nyani,
Unasema una nini?
Siyo rafiki, una koboko!

Ukiwa naye rafiki ....
Umualikaye mloni, mkala vyakula vya tani,
Huku mkicheka vinywani, na kwa mwingi mno utani,
Mkawa mumo furahani, si mchana wala jioni,
Milo mwatia matumboni, ya manyama na biriani,
Na akiondoka nyumbani, akusema huna maani,
Unasema una nini?
Ni rafiki wa kitambi!

Ukiwa naye rafiki ...
Ajidhaniye kwa Mungu, alokuja ulimwenguni,
Akutoe kwenye mvungu, na akuweke hadharani,
Akuone kama mkungu, uloanguka mchangani,
Kwamba bila ya yeye mungu, ni bure hunayo thamani,
Tena ayapike majungu, wajua jamaa fulani,
Mimi ni kama wake mungu, bila mimi yeye ni duni,
"Nimemuopoa mvungu, alizamia matopeni."
Unasema una nini?
Siyo rafiki, sheitwani!

Ukiwa naye rafiki ....
Ukamfichulia siri, mnapokaa kikaoni,
Wa kuenda naye safari, mpite hata na porini,
Mfano waenda mandari, mkisurura moyoni,
Na wewe kwa yako suduri, kabisa unamuamini,
Na tena dhahiri shahiri, ukamueleza kinywani,
Kisha mkiwa kwenye pori, wawili mmezama ndani,
Anakupiga na kabari, huku akuita mwandani,
Akikugeuza bakari, wewe kutiwa kisu shingoni,
Huku akiona fahari, akikuhasiri mwilini,
Unasema una nini?
Siyo rafiki, mumiani!

(Limenukuliwa kutoka Diwani ya Kaza Macho*)*

(a) Fafanua kwa hoja sita ujumbe unaojitokeza katika shairi hili. (alama 6)
(b) Bainisha vipengele vitatu vya kimtindo vilivyotumiwa katika ubeti wa nne wa shairi hili. (alama 3)
(c) Onyesha aina tatu za uhuru wa kishairi katika shairi hili. (alama 3)
(d) Bainisha nafsineni ya shairi hili. (alama 2)
(e) Eleza toni katika shairi hili. (alama 2)
(f) Andika ubeti wa kwanza kwa lugha ya nathari. (alama 4)

7. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

Tulapo
Nyama kwa wingi,
Kubugia mapande mengi,
Tukapukuta magombe mengi,
na kutafarahi kwa wingi,
tena kiburi kingi,
kwamba
tupo kileleni,
kwa shehena ya tumboni,
na furaha ya kinywani,
Tukijibweteza kochini,
Pasi mazoezi mwilini,
Hatuli ...
Twaliwa.

Tubugiapo ...
chipsi na kaukau,
Na keki kuzikakatua,
Na peremende kuzibanjua,
Na vinywaji vya sukari,
Tuk'amba na kujigamba,
Vina utamu gegoni,
Vinatushuka tumboni,
Tukajilaza masebuleni,
Na popoo zetu runingani,
Mwenendo wa hizi zamani,
Hatuli ...
Twaliwa.

Tuizapo
Mboga zetu za majani,
Tena za toka zamani,
Kurarambukia za madukani,
Zitokazo viwandani,
Ili tuwe tu safuni,
Usasa twamanya nini,
Hatuli ...
Twaliwa.

Tuchukiapo
viazi vitamu, mayugwa na muhogo,
Kisamvu tukakicha kama mbogo,
Tusile japo kidogo,
Tutape yenye uto milo,
Ili nasi tuwe tumo,
Twajua kwenda na wakati,
Hatuli ...
Jama hatuli, twaliwa.

Twaliwa
na
Baulisukari,
Twaliwa na jongo,
Twaliwa na unene,
Twaliwa na utepetevu,
Twaliwa na wakati,
Twaliwa na ukengeushi,
Twaliwa jama twaliwa.

(K. K. Wamitila)

(a) Eleza ujumbe katika shairi hili. (alama 6)
(b) Fafanua umuhimu wa aina mbili za urudiaji katika ubeti wa kwanza wa shairi hili. (alama 4)
(c) Bainisha aina zifuatazo za uhuru wa kishairi katika shairi hili: (i) inkisari (ii) utohozi (alama 2)
(d) Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 2)
(e) Eleza toni katika shairi hili. (alama 2)
(f) Andika ubeti wa tatu kwa lugha ya nathari. (alama 4)

Sehemu E: Fasihi Simulizi

8. Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali.

Hapo zamani za kale paliishi mzee mmoja kwa jina Mutangilu. Mutangilu alipenda nyama kupindukia. Kukiwa na hafla kama vile arusi, alihakikisha kwamba alihudumu katika upishi wa nyama. Siku moja alikula nyama kukithiri mpaka akashindwa kutembea kurudi nyumbani. Vijana wanne walimshika na kumweka kwenye toroli na kumsukuma wakimpeleka nyumbani.

Hawakuwa wamesukuma toroli zaidi ya kilomita moja wakati walivamiwa ghafla na harufu mbaya mithili ya makwapa ya sokwe. Mara, tumbo la Mutangilu likanguruma kama radi na wote wakashtuka. "Nisaidieni, nataka kujisaidia," Mutangilu akasema huku akitokwa na kijasho kinene.

Kwa bahati nzuri, karibu na barabara palikuwa na msala. Vijana walisukuma toroli kwa kasi na kumzoa Mutangilu karibu na msala. Salala! Yaliyofuata hayaambiliki, hayasemezeki. Vijana walimwacha Mutangilu na kutoroka kwa yale waliyoyaona, waliyoyasikia na waliyonusa.

Wiki mbili hazikupita kabla ya Mutangilu kuhusika katika kisanga kingine. Aliingia katika buruji la kondoo wake na kumbeba kondoo mmoja hadi kichakani. Alichukua ngozi ya fisi na kumgubika yule kondoo. Kondoo alionekana kama fisi, shilingi kwa ya pili. Alirudi nyumbani haraka na kumwita mke wake. "Mandalina, Mandalina ... hebu njoo uone maajabu! Fisi amemla kondoo wetu na halafu akakwama pale kichakani akitoroka."

Mandalina alimfuata mume wake kujishuhudia. Alimwona fisi aliyekwama kichakani.

"Ingawa mila zetu hukataza kula nyama ya fisi, hazijatukataza kumchinja," Mutangilu akasema na kumchinja fisi.

"Ingawa mila zetu zimetukataza kumla fisi, hazijatukataza kuchuna ngozi yake," akasema na kuchuna ngozi.

"Ingawa mila zetu zimetukataza kumla fisi, hazijatukataza kumkatakata vipande," Mutangilu akasema na kukatakata nyama.

"Turudi nyumbani nikuandalie chakula mume wangu," Mandalina akamwambia mume wake.

Mutangilu alisitasita lakini mwishowe akakubali shingo upande. Mandalina alimwandalia mumewe chakula na kisiri akarudi mbio pale kichakani. Alibeba nyama kwa mifupa na kuzipeleka jikoni bila kuonekana na yeyote. Mutangilu alirudi kichakani tayari kuoka nyama ile kisiri, lakini wapi? Alipata ngozi ya fisi pekee. Familia ya Mutangilu ilikula nyama ya kondoo kwa siku tano mfululizo! Hadithi yangu inaishia hapo!

(a) (i) Toa sababu tatu kuonyesha kwamba hadithi hii ni hekaya. (alama 3)
(ii) Fafanua vipengele sita vya kimtindo vilivyotumiwa kuwasilisha hadithi hii. (alama 6)
(iii) Eleza shughuli tano zinazotambulisha utamaduni wa jamii hii. (alama 5)
(b) Eleza changamoto sita zinazoweza kumkumba mkusanyaji wa data ya Fasihi Simulizi akitumia kamera ya kunasa video. (alama 6)

More Kiswahili papers