KCSE Revision AI kcserevision.app

KCSE 2023 Kiswahili Paper 2

The KCSE 2023 Kiswahili Paper 2 (102/2). Ufahamu, ufupisho, matumizi ya lugha na isimujamii. View it below, download it to print, or revise it with the AI tutor, which takes you through each question and marks your answers. Source: Teacher.co.ke.

102/2 · KISWAHILI · Karatasi 2 · Nov. 2023 · 2½ saa

Maagizo: Jibu maswali yote. Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

1. Ufahamu (alama 15)

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Timo alitunukiwa zawadi ya simu na kaka yake baada ya kuhitimu kidato cha nne. Hii ni zawadi ambayo hakuitarajia, japo alitamani kuwa na simu yake kwa miaka mingi. Alifurahi ghaya. Hata hivyo, kaka yake alimshauri kuhusu namna ya kutumia simu ya mkononi kwa uangalifu. Mbali na hayo, alimtahadharisha kuhusu madhara ya kuitumia kiholela.

"Sasa nina ulimwengu mzima mkononi mwangu. Nitafaidi mengi kutokana na kifaa hiki." Timo alijiambia kimoyomoyo. Mwanzoni, Timo alizingatia ushauri aliopewa na kaka yake huku akitekeleza majukumu yake ipasavyo. Alifurahia kutumia simu yake kwa kupiga picha, kutuma na kupokea ujumbe, kusikiliza muziki, kuangaza chumba chake usiku, na kuwasiliana na marafiki. Kadri mawasiliano na marafiki wake yalivyoimarika, ndivyo alivyozinduliwa kuhusu matumizi zaidi ya simu. Hatimaye aliambua kuwa simu yake ilikuwa na Facebook, Twitter, WhatsApp, Instagram na Tiktok.

Timo alianza kuzuzuliwa na mitandao hiyo mipya ya kijamii. Simu yake haikubanduka mikononi mwake. Hakutofautisha tena kati ya mchana na usiku. Hata muda wa kula na kuoga alikosa. Simu ilimgeuza jongoo akawa haoni mbele wala nyuma. Uraibu huu wa simu ya mkononi uliwatia wengi simanzi. Walioshangazwa zaidi ni wazazi wake na kaka yake aliyemnunulia simu hiyo. Walimrai aache tabia hiyo hasi. Rai zao ziliangukia sikio la kufa lisilosikia dawa.

"Mwanangu, kila nikikukanya kuhusu simu yako ya mkononi, unanipuuza na kununa. Simu imekuteka nyara. Huna muda wa kufanya shughuli zako wala wa kujumuika na familia." Mama angemkumbusha kila mara.

"Mama, simu hii ina matumizi mengi. Huoni vile wanamuziki wanavyotumbuiza kwenye YouTube? Huoni wanasarakasi na vioja vyao, hata nyimbo za dini … Siku hizi kila kitu kinafanyika kwenye simu." Timo angejitetea. "Hata kazi ni mumu humu. Ulimwengu umebadilika eti!" Timo angesisitiza.

Mienendo ya Timo ilizidi kumpa mama yake wasiwasi. Baba yake naye, akaamua kutenga muda azungumze na mwanawe.

"Timo, huko mitandaoni mwingiako kuna faida gani ikiwa hamfanyi utafiti na kuvumbua mambo mapya? Ni hasara kubwa kuwa mtumizi tu." Baba alimuasa. Timo aliinamisha kichwa na kuondoka pole pole hadi chumbani mwake. Haikumjia akilini kwamba ameshakuwa mraibu wa simu. Siku hiyo, hakutoka chumbani. Alishangazwa na malalamishi ya wazazi wake, kimbilio likawa ni marafiki aliowafahamu na wengine wengi asiowafahamu mtandaoni.

Simu ya mkononi ilimhini Timo mengi. Alikuwa katika ulimwengu wake. Alipitwa na mengi; alikosa kujumuika na vijana wenzake maabadini, michezoni na katika shughuli nyingine za vijana. Mambo aliyoyatazama mtandaoni yalimpumbaza. Aliota usiku na mchana. Alijenga makasri hewani, akaingiwa na tamaa ya kutajirika haraka kutokana na visa alivyovisoma na video alizotazama. Kila uchao ungemsikia akiwasimulia rafiki zake jinsi alivyotarajia kutajirika. Alijigamba, "Hivi karibuni nitatambulika kote. Nitakuwa mshawishi mkubwa ajabu kwenye tasnia ya mitandao ya kijamii. Nitapiga picha na kurekodi video za vichekesho na kutuma kwenye mitandao ya kijamii. Watu watazipenda na kuzisambaza picha na video zangu. Nitapata pesa nikiwa nimekaa hapa tu."

Ndoto ya Timo ilibaki kuwa ndoto tu. Hakufanya lolote ili kuitimiza. Hata mpango aliokuwa nao wa kuweka picha na video mtandaoni haukutimia, akawa mtazamaji badala ya mshiriki. Habari za wengine mtandaoni zilizalisha kicheko kisichoeleweka. Kila aliyemwona Timo alidhani ni mwehu. Ilibidi familia yake kuingilia kati. Wazazi walitafuta mshauri. Baada ya mshauri kumkagua Timo, ilibainika kwamba alihitaji kupelekwa kwenye kituo cha kurekebishia tabia. Lilikuwa pendekezo zuri ila lingewagharimu wazazi wake Timo.

Timo hakushawishika na pendekezo la mshauri. Hata hivyo, baada ya ushauri wa wazazi na marafiki waliomjali, akakubali. Miezi mitatu baada ya Timo kuwa kituoni, ripoti walizozipata wazazi zilikuwa chanya. Timo alikuwa tayari kufungua ukurasa mpya wa maisha yake.

(a) "Matumizi ya simu bila tahadhari yana athari kwa mtumiaji." Thibitisha kwa hoja tano kutoka kwenye kifungu. (alama 5)
(b) Fafanua kwa hoja nne, juhudi zilizowekwa ili kumsaidia Timo kutoka kwenye tatizo lililomkabili. (alama 4)
(c) Eleza mtazamo wa: (i) wazazi kuhusu tabia ya Timo; (alama 2) (ii) Timo kuhusu matumizi ya simu. (alama 2)
(d) (i) Andika maana ya 'imekuteka nyara' kwa mujibu wa kifungu. (alama 1) (ii) Andika kisawe cha 'simanzi' kulingana na kifungu. (alama 1)

2. Ufupisho (alama 15)

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Katiba ya Kenya imetoa mwongozo kuhusu namna masuala ya kijamii yanavyopaswa kushughulikiwa kisheria. Miongoni mwa sheria hizo ni ile inayohusu suala la ugavi, umiliki na urithi wa mali katika jamii. Sheria hii inasisitiza pawe na usawa katika umiliki wa ardhi. Katika utekelezaji wa sheria hii, kipengele cha usawa wa kijinsia kimepewa kipaumbele katika katiba Sura ya 5, Kipengele cha 1(f). Kipengele hiki kinaelekeza kumalizwa kwa ubaguzi wa kijinsia katika jamii. Licha ya sheria kuwa bayana, baadhi ya wanawake nchini Kenya wamenyimwa haki ya kurithi ardhi na mali kutoka kwa wazazi wao. Hili linadhihirika kutokana na mizozo ya mara kwa mara inayoshuhudiwa na kuripotiwa katika vyombo vya habari.

Imani za kitamaduni zimechangia hali hii inayomnyima mwanamke nafasi ya kumiliki, kusimamia na kudhibiti mashamba na aina nyingine za mali katika jamii. Mathalani, ripoti iliyotolewa na Shirika la Human Rights Watch, inaangazia kauli za baadhi ya wanajamii kuhusu umiliki wa mashamba. Kulingana nao, mwanamume ndiye mwenye mamlaka katika ndoa, hivyo ndiye anayepaswa kumiliki mali, yakiwemo mashamba. Katika hali hii, ni dhahiri kuwa mwanamke hubakia tu kuiongezea thamani mali hiyo, ama kwa kulima, au kushiriki katika shughuli nyingine za kuzalisha mali.

Suala la mwanamke kutomiliki mali linaongozwa na imani kuwa mtoto wa kike huolewa huku wa kiume akibaki. Inaaminika kwamba, huko anakokwenda, mtoto wa kike atafaidika kwa shamba la mumewe. Hivyo, akimiliki shamba la wazazi, atanufaika maradufu. Kwa upande mwingine, mtoto wa kiume asipomiliki na kudhibiti mali kwao, huenda akahisi kuwa amedhulumiwa.

Juhudi za wanawake za kupigania umiliki wa mashamba zinakabiliwa na changamoto anuwai. Wapo wanawake wengine wanaoogopa kutoa sauti kuhusu hali ya kunyimwa haki ya kurithi kwa kuchelea kunyanyaswa zaidi. Baadhi yao hawana ufahamu kuhusu haki zao za kurithi ardhi na mali. Huenda pia walinyimwa nafasi ya kupata elimu. Hata wale walio na ufahamu, hukabiliwa na gharama ya kuwasilisha kesi kortini. Haya husababishwa, ama na ada ya wakili, au umbali wa taasisi za kisheria kutoka kwa wahusika.

Isitoshe, migogoro ya kifamilia wakati mwingine huchelewesha utekelezaji wa uamuzi wa mahakama. Itokeapo kwamba, mmoja wa wanafamilia atapinga uamuzi wa mahakama kuhusu ugavi wa mali, huenda mhusika akahitajika kukata rufaa na kuafikiana. Si ajabu kwamba kesi nyingi kuhusu umiliki wa mali na mashamba zimeselelea mahakamani bila kukatiwa hukumu.

Ipo haja ya wanajamii katika ngazi zote kuweka mikakati ifaayo kuhakikisha kwamba mwongozo unaotolewa kuhusu umiliki wa mashamba na mali umetekelezwa. Hususan viongozi na wanajamii walio na mamlaka ya kuendeleza utekelezaji wa sera wanahitaji kufanya kazi bega kwa bega na wanajamii mashinani ili kuzuia dhuluma katika ugavi wa mali na mashamba. Taasisi na mashirika yanayohusika na masuala ya kisheria na kijamii yawaelimishe na kuwahamasisha raia kuhusu kutobagua mtoto katika kurithi na kumiliki mali.

(a) Fupisha ujumbe wa aya tatu za kwanza. (maneno 90) (alama 8) (Matayarisho / Nakala safi)
(b) Fafanua masuala ambayo mwandishi anaibua katika aya tatu za mwisho. (maneno 70) (alama 7) (Matayarisho / Nakala safi)

3. Matumizi ya Lugha (alama 40)

(a) Sauti /b/ katika neno bora ni kipasuo cha midomoni. Andika sifa mbili za sauti iliyoandikwa kwa herufi nzito: **ng'**oa. (alama 1)
(b) Bainisha silabi katika neno lifuatalo: tunza. (alama 1)
(c) Ainisha mofimu katika neno lifuatalo: mlizoleta. (alama 2)
(d) Andika sentensi ifuatayo upya kwa kubadilisha neno lililopigiwa mstari kuwa nomino: Barabara nzuri ziliufanya mji uvutie. (alama 2)
(e) Andika upya sentensi ifuatayo ukitumia ki ya masharti: Juma angekamilisha mradi huo mapema, angekihakikishia kijiji chake usalama wa chakula. (alama 2)
(f) Akifisha sentensi ifuatayo: ajabu mwezi wa januari una mvua (alama 2)
(g) Ainisha maneno katika sentensi ifuatayo: Mwenye bidii atatuzwa hadharani. (alama 1)
(h) Andika sentensi ifuatayo katika wakati uliopita hali timilifu: Vyumba katika bweni lile vinapakwa rangi. (alama 2)
(i) Bainisha kirai kivumishi na kirai elezi katika sentensi ifuatayo: Mwanafunzi yule mwadilifu alifika mapema mno. (alama 1)
(j) Andika sentensi ifuatayo katika hali ya ukubwa: Barabara hizi zilikarabatiwa mwaka jana. (alama 1)
(k) Bainisha matumizi mawili ya -po- katika sentensi ifuatayo: Maria hushangiliwa sana anapoimba. (alama 2)
(l) Andika upya sentensi zifuatazo kulingana na maagizo.
 (i) Wanakijiji walifika kwa wakati kuzoa taka. Gari la kubeba taka lilichelewa. (Unganisha kwa kutumia 'ingawa'.) (alama 2)
 (ii) Katana alichukua stakabadhi zote zilizohitajika, akazitia kwenye faili. (Kanusha.) (alama 2)
 (iii) Rita alimrai Waridi amfunze kucheza kandanda. (Tumia kisawe cha neno lililopigwa mstari.) (alama 1)
(m) Tunga sentensi yenye vishazi viwili huru. (alama 2)
(n) Kiambishi wa katika kitenzi wanasaidia kinaonyesha mtenda. Tunga sentensi yenye kiambishi ku cha yambwa. (alama 2)
(o) Andika upya sentensi zifuatazo kwa kuzingatia maagizo.
 (i) Helikopta iliyobeba wanajeshi hao ilipaa angani saa tano asubuhi. (Andika kinyume cha maneno yaliyopigiwa mstari.) (alama 2)
 (ii) Vyumba vya kurekodia nyimbo vina mwangwi. (Andika katika umoja.) (alama 2)
 (iii) Kanini aliwapikia pilau watoto wa Aisha. (Anza kwa: Watoto …) (alama 2)
(p) Angua ni tendo la kutoa matunda mtini; angua pia ni: (alama 2)
(q) Tunga sentensi ukitumia kwa kuonyesha nia. (alama 2)
(r) Nomino bidii imo katika ngeli gani? (alama 1)
(s) Robota ni kwa pamba, tita ni kwa ……… na ……… ni kwa blanketi. (alama 2)
(t) 'Haba na haba hujaza kibaba' ni methali inayotumiwa kuonyesha umuhimu wa kuthamini na kuvihifadhi vitu vichache tulivyo navyo kwa kuwa vikiwekwa pamoja huwa vingi, vikakidhi haja. Andika methali unayoweza kutumia kumhimiza mwenzako kutenda mambo mazuri. (alama 1)

4. Isimujamii (alama 10)

Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.

Msemaji 1: Hii ni booster inayotolewa ili kuimarisha kinga dhidi ya virusi hivi. Je, ulipata dozi ya kwanza na ya pili?
Msemaji 2: Naam, zote mbili.

(a) Bainisha sajili ya mazungumzo haya. (alama 1)
(b) Eleza sifa tatu za sajili hii kwa kurejelea makala haya. (alama 3)
(c) Eleza sifa nyingine sita ambazo hutambulisha sajili ya aina hii. (alama 6)

More Kiswahili papers