KCSE Revision AI kcserevision.app

KCSE 2024 Kiswahili Paper 2

The KCSE 2024 Kiswahili Paper 2 (102/2). Ufahamu, ufupisho, matumizi ya lugha na isimujamii. View it below, download it to print, or revise it with the AI tutor, which takes you through each question and marks your answers. Source: Teacher.co.ke.

102/2 · KISWAHILI · Karatasi 2 (Lugha) · Nov. 2024 · Saa 2½

Maagizo: Jibu maswali yote. Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

1. Ufahamu (alama 15)

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Kule kijijini kwetu tulipenda sana kuwakaribisha wageni na hasa ndugu zetu waliofika kwa ajili ya kujipumzisha wakati wa likizo. Tulipenda kuwadadisi na kuwaweka katika mizani. Nani kanunua gari? Nani kaoa? Nani ana suti nzuri? Hakika maswali yetu yalikuwa mengi sawa na majibu tuliyopata. Wajua tena kila mmoja wetu alijikatia kauli kuhusu nani kapiga hatua maishani na nani hakupiga. Hiki kilikuwa kipindi cha gumzo zisizoisha kijijini. Siku moja, baada ya shughuli za kutwa, tulikaa chini ya mti mmoja mkubwa kwa ajili ya soga kama ilivyokuwa ada walipofika watu kutoka mjini. Sikumbuki ilitokeaje lakini mara nilisikia sauti ya mama ikieleza huku kila mmoja ametulia.

"Afadhali likizo iishe tupate amani. Ndugu zetu hawa wamekuja na kukifanya kijiji kuwa chao. Sijui hatujui kufanya nini! Sijui nani anaendelea vipi! Eti yuko pale pale. Sielewi …"

"Wewe nawe! Hivi huna kazi? Kazi imekuwa kunusa nani ana nini? Sasa haya yanakuhusu nini? Utamaliza visigino bure kwa safari za umbeya," alitoa dukuduku lake Shangazi Kwini.

Tulibaki tumezubaa kiasi. Hakuna aliyethubutu kutoa kauli yake hadi pale Yeni aliposema, "Lakini, shangazi, hivi huoni? Juzi nimekwenda sokoni. Unadhani ni nini sikuona? Haya macho yaliona maajabu. Wamekuja mabinti na viguo kama sijui nini. Na vyenyewe hivyo viguo ni kama miwani; vyaona mpaka ndani. Unashindwa kama kweli kuna maana ya kuvaa."

Kauli hii kama ilipiga jeki azma ya Muna kutaka kusema. Mara naye alieleza, "Yeni, Shangazi Kwini karibu aniue bilashi ilhali ukweli wenyewe huo kama uyoga umejidhihirisha. Wangapi wamerudi baada ya mwaka tu kule nje lakini leo ukiwasemesha kwa lugha yetu ya asili wanakwepa na kujibu kwa lugha ya kigeni? Hawa wenzetu wanajua wazi kuwa hapa kuna wengi ambao lugha ya kigeni inawapita kama upepo kwenye viganja. Wengi wamekuja na kudai hawali tena mchicha au mrenda. Jana tukivila nao hapa! Kama si unafiki huo ni nini?"

Muna alisema haya na kuwaacha waliokuwepo wanacheka na kushangilia. Ni kama waliopata fursa kulipiza kisasi ambacho sasa kilikuwa siri kubwa.

"Hawa basi," alisema shangazi Kwini. "Kama wanafanya yote hayo inatuuma kwa nini? Uwike usiwike kumbuka kutakucha. Kukicha hiyo kesho, tutakuwa tumeambua nini? Hadithi?"

Haya yaliposemwa, mwanamke mmoja aliyekuwa ameketi pale kimya muda wote huu aliinuka. Alisafisha koo kabla ya kujieleza.

"Afadhali wasemwe. Labda itasaidia. Wamekuja kwa fujo mpaka hatupumui kama zamani. Wanajitia ujuzi wa kila kitu. Hivi sisi hapa hatujui kitu?" Aliuliza huku anashangiliwa kwa makofi na vifijo. Lakini hakutaka mazungumzo yake kukatwa. Alisema, "Mtazame Bwana Tambo. Yeye ana kazi huko. Si kama sisi. Amekuja likizo kupumzika. Badala ya kupumzika amekuja hapa kufanya kazi tunayofahamu sisi kufanya. Kishamba cha mboga anapalilia yeye. Ng'ombe anawatafutia yeye majani na analengeta yeye. Hata kazi ya kuosha vyombo hatuwezi kuitiwa. Sasa mtu kama huyu tukisema ni bahili mtasema ni umbeya? Halafu kuna wengine ambao kuwasalimu ni kero. Unampa mkono unaona anataabika kuupangusa wake kwenye nguo baada ya salamu."

Sasa mazungumzo yalikuwa yamenoga; kila mmoja wetu alikuwa amevutwa nayo kama msumari unavyovutwa na sumaku. Hata hivyo, nilipokumbuka mazungumzo yangu na Bwana Tambo niliona kama anachokozwa kwa kilicho chake. Kazi ile inayomletea lawama ni yake na anayeifanya si mwingine bali ni yeye. Nilikumbuka aliyoniambia siku moja nilipoenda kwake.

"Watu wengi hufikiri wakati wa likizo ni kipindi cha kulaza damu kwa kujimwaya kwenye makochi. Hiki ni kipindi muhimu cha sisi wenye kazi za afisi kuusaidia mwili kufanya kazi. Kazi hizi huifanya misuli kuimarika na ubongo kuchangamka. Mwisho wa likizo unajikuta umo katika hali nzuri ya kuanza tena kazi afisini. Kwa kufanya kazi, viungo huhisika kuwa vyepesi. Aidha kwa kufanya kazi hizi tunabaki kujikumbusha asili yetu. Zinaleta picha hai ya jana zetu katika maisha yetu," alinieleza Bwana Tambo.

(a) Eleza mitazamo ya watu wa mjini kuhusu watu wa kijijini kulingana na kifungu. (alama 2)
(b) Onyesha jinsi tabia za watu wa mjini zilivyowaathiri watu wa kijijini. (alama 5)
(c) Fafanua manufaa manne ya likizo kama inavyodhihirika kwenye kifungu. (alama 4)
(d) Bainisha sifa mbili za msimulizi wa kisa hiki. (alama 2)
(e) Eleza maana za maneno haya kulingana na kifungu: (i) alijikatia kauli; (ii) yamenoga. (alama 2)

2. Ufupisho (alama 15)

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Muziki una nafasi kubwa na muhimu katika maisha ya watu. Nguvu za muziki hazimithiliki na chochote japo aghalabu hatuoni hivyo. Hebu fikiria ulimwengu ungekuwa vipi bila muziki. Labda mwanadamu asingekuwa na njia mbadala ya kujieleza wala asingefaidi uhondo unaoletwa na sanaa ya muziki!

Njia mojawapo kuu ya mwanadamu kujiburudisha ni kupitia kwa muziki. Burudani ya muziki si ghali na inaweza kufikiwa kwa njia mbalimbali. Vyombo vya kiteknolojia kama vile redio na runinga hurusha na kupeperusha mahadhi ya muziki kupitia kwa mawimbi. Kubuniwa kwa kadi sakima, diski mweko na vifaa vingenevyo vya kuhifadhi muziki kumeleta afueni kubwa kwa maashiki wa muziki. Sasa imekuwa rahisi kuhifadhi na kusambaza muziki ambao awali ulikuwa adimu. Kwa hivyo, si ajabu tena kukutana na mtu akiwa mbioni kuchapa kazi zake huku anasikiliza muziki. Wapo wengine wanaosikiliza muziki wakiwa wanasafiri katika vyombo kama vile gari, ndege na pikipiki.

Watu wengi, hasa katika sehemu za mji, hupenda kujiburudisha katika maeneo yenye muziki mtamu unaoweza kumtoa nyoka pangoni. Hapa utawaona wanamuziki wakiwa wamezama katika usanii wao na kuziachilia nyimbo moto moto zinazowafanya watu kuchezesha vichwa vyao na kugotagota meza bila kufahamu kuwa wameisha kutwaliwa na nguvu za uchawi wa muziki. Wengine hujikuta wamesimama kwa kuitikia wito wa gitaa na kuanza kunengua viuno vyao. Hiki huwa kipindi cha kuburudisha na pengine kumvua mtu huzuni. Nao wapiga muziki hufurahi kwa namna watu wanavyoipokea sanaa yao. Zaidi ya furaha hii, wasanii huchuma katika mazingira haya. Muziki huwapa ajira ambayo huwaletea kipato cha kujikimu na kuziendesha familia zao. Wasanii hawa kwa kufahamu nguvu za muziki, wanazigeuza talanta zao kuwa kitegauchumi.

Ingawa idadi kubwa ya watu huhusisha muziki na burudani, hapana shaka kwamba muziki ni nyenzo kuu ya kutolea mawaidha. Waumini wa dini mbalimbali hutunga nyimbo zenye mawaidha na kuzitumia ndani na nje ya maeneo yao ya ibada. Nyimbo za ibada huitangaza dini hata bila watu kujumuika pamoja au kuwa wa dini moja. Vivyo hivyo, nyimbo zisizo za dini hubeba mawaidha mbalimbali. Lengo huwa ni kuipa jamii mwelekeo ufaao. Kuna miziki inayohusu mapenzi, unyumba, malezi, maadili miongoni mwa jumbe nyingine murua kwa ajili ya jamii. Miziki hii vilevile huwa hifadhi ya utamaduni wa watu na balozi mwema wa utamaduni huo.

Jambo la kuvunja moyo ni kuwa, zipo dalili za kudorora na kufa kwa muziki. Wanamuziki wa awali walijijengea umahiri wa kucheza vyombo mbalimbali vya muziki. Ustadi wa kupiga vyombo vya muziki uliwaacha hoi wapenzi wa muziki. Wasanii hawa walionyesha ustadi wao kwa mbwembwe kuu kwa maana walijiamini. Wasanii wengi wa kisasa hawajizingatii upigaji vyombo vya muziki. Badala yake wanategemea midundo iliyorekodiwa ya zana za muziki. Wanamuziki hawa huingia kwenye studio na kurekodi nyimbo zao kwa kufuatilizia midundo iliyorekodiwa. Tatizo lililopo ni kuwa, katika siku za halafu hapatakuwa na wajuzi wa zana zetu za muziki. Matokeo yake ni kuwa hatutaweza kuwapokeza chipukizi wanaojiunga na tasnia ya muziki maarifa waliyoyajenga watangulizi wetu.

Suala lingine linaloashiria kudumaa kwa muziki wetu ni haraka ya wasanii wetu wenye hamu kuu ya kutoa nyimbo haraka. Nyimbo za haraka zinakosa umakinifu wa ujumbe wa usanii. Zipo nyimbo ambazo hazikumakinikiwa vya kutosha. Nyimbo hizo zinakosa uwiano mzuri wa ala za muziki na mawazo. Utaona kuwa kuna nyimbo ambazo zinakosa heshima. Muziki, sawa na sanaa nyingine, unafaa kujali hadhira inayoupokea. Kuitia aibu hadhira kwa kusikiliza muziki usio wa heshima ni kuiadhibu. Hadhira inayoadhibiwa huona muhali kuushabikia muziki utoao adhabu. Kwa ufupi, nyimbo hizi zilizozalishwa kwa haraka vilevile hukumbana na kifo cha mapema mikononi mwa hadhira inayofaa kuwa mlezi wazo.

(a) Fupisha aya nne za kwanza kwa maneno 100. (alama 9)
(b) Eleza ujumbe unaojitokeza katika aya mbili za mwisho kwa maneno 70. (alama 6)

3. Matumizi ya lugha (alama 40)

(a) Andika neno lenye kitamkwa cha ufizi. (alama 1)
(b) Onyesha silabi inayotamkwa kwa mkazo katika neno: uliopandwa. (alama 1)
(c) Eleza majukumu ya viambishi katika neno: vikimvutia. (alama 2)
(d) Andika upya sentensi zifuatazo kwa kufuata maagizo. (alama 8)
 (i) Mabaharia walifika bandarini. Walikuwa wamesafiri kwa wiki moja. (Unganisha kuwa sentensi moja kwa kutumia kiunganishi cha wakati.)
 (ii) Mkurugenzi alimpandisha cheo afisa husika ambaye alivumbua huduma hiyo. (Andika upya sentensi kwa kugeuza kitenzi kilichopigiwa mstari kuwa nomino bila kubadilisha maana.)
 (iii) Wanakijiji wataweka mikakati ifaayo. Watajitosheleza kwa chakula. (Unganisha kuunda sentensi changamano.)
 (iv) Barabara hiyo itapitia Shazi. (Kanusha kwa kuanza kwa neno: Shazi…)
(e) Tunga sentensi zenye vihisishi vinavyoibua hisia zifuatazo: (i) kinyume cha matarajio; (ii) kutaka kitu kinusurike. (alama 2)
(f) Andika sentensi ifuatayo katika kauli ya umoja: Makasha hayo yaliyotengenezewa viwandani na mafundi hao yaliwanufaisha. (alama 2)
(g) Geuza sentensi ifuatayo katika hali ya ukubwa: Nguo zenyewe zilihifadhiwa kwenye vikapu. (alama 1)
(h) Tunga sentensi katika wakati uliopo kuonyesha kwamba kitendo kimekuwa kikiendelea kwa muda. (alama 1)
(i) Andika upya sentensi ifuatayo kwa kuanza kwa yambwa tendwa: Vijana walisafisha soko la kijiji chao. (alama 2)
(j) Geuza sentensi ifuatayo katika usemi halisi: Chifu aliwakumbusha walezi kwamba walihitaji kuwapeleka watoto kwa chanjo dhidi ya polio Ijumaa ambayo ingefuata. (alama 2)
(k) Bainisha maana tatu katika sentensi ifuatayo: Mandila aliwatangazia chao. (alama 3)
(l) Kistari kifupi hutumiwa kutenga silabi. Vilevile, huweza kutumiwa kudokeza hoja. Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mengine mawili ya kistari kifupi. (alama 2)
(m) Tunga sentensi yenye muundo ufuatao: KN(N+V) + KT(T+KH) + U + KN(Ø) + KT(T+E) (alama 2)
(n) Bainisha matumizi ya kwa katika sentensi: Kuhamia kwa jamii hiyo kulisifiwa na wengi; wenyeji kwa wageni. (alama 2)
(o) Nomino zifuatazo zimo katika ngeli gani? (i) mafuta; (ii) kwato. (alama 2)
(p) Tumia nahau badala ya maneno yaliyopigiwa mstari: Tuta aliwaomba msamaha wazazi wake. (alama 1)
(q) Kusimulia ni kwa kutamba, ______ ni kwa adabu na ______ ni kwa imara. (alama 2)
(r) Methali jifya moja haliinjiki chungu huambiwa mtu ambaye haoni umuhimu wa kushirikiana na wengine. Ni methali ipi ambayo huambiwa mtu ambaye anadharau vitu duni ambavyo vinaweza kumfaa wakati wa shida? (alama 1)
(s) Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya kazi na kasi. (alama 2)
(t) Jirani yako ameshukiwa kufanya kosa na kutiwa ndani. Atalipa ______ ili kuachiliwa kwa muda kesi ikisikilizwa. (alama 1)

4. Isimujamii (alama 10)

Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.

Mpenzi mteja, wakati wa kurudi shule umefika nayo mahitaji yamekujaa pomoni? Usijikune kichwa bure!

Tazama jinsi kurudi shule kulivyorahisishwa! Ni kama kumeza mate tu. Rafiki yako, Shirika la Jiimarishe, amekuzindulia mpango murua. Mpango unaojali watoto wako. Mpango unaojali mfuko wako. Mpango wa kukusuluhishia matatizo yako yote. Pata karo ya shule bure! Pata shopping bure! Huhitaji kutoa hata tone moja la jasho. Unachohitaji ni kubonyeza vitufe vya rununu yako ukiwa hapo hapo sebuleni mwako; kwenye kochi lako na utaona muujiza wa mkopo ambao ni kama unapewa bure! Absolutely free!

(a) Bainisha sajili ya makala haya. (alama 2)
(b) Fafanua sifa nane za sajili hii kwa kurejelea makala haya. (alama 8)

Marking scheme

Loading…

More Kiswahili papers