102/3 · KISWAHILI · Karatasi 3 (Fasihi) · Nov. 2023 · 2½ saa
Maagizo: Jibu maswali manne pekee. Swali la kwanza ni la lazima. Maswali mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki, yaani Riwaya, Tamthilia, Hadithi Fupi na Fasihi Simulizi. Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
Sehemu A: Ushairi
1. (Lazima) Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
1. Hima nakuja jamani, muanga kuwatolea,
Kwani ninayo imani, ni wengi wamepotea,
Kwa hiyo nawaombeni, niruhusuni kwongea,
Elimu nawambieni, kwamba haina kikomo.2. Elimu yawatolea, mwajua ni kitu gani,
Elimu ukipokea, utakuwa thawabuni,
Kitu gani nasemea, fikirini jijibuni,
Elimu nawambieni, kwamba haina kikomo.3. Kaya unapoachia, unaingia shuleni,
Jama mkifikiria, kweli huko ni kazini,
Hesabuni waingia, na kusoma nyingi fani,
Elimu nawambieni, kwamba haina kikomo.4. Tangu ukiwa nyumbani, elimu unaanzia,
Kule kunawa usoni, nalo somo angalia,
Kuna mafunzo jandoni, na huko kumbini pia,
Elimu nawambieni, kwamba haina kikomo.5. Unapotoka shuleni, ulimwenguni wangia,
Usipofunzwa nyumbani, utafunzwa na dunia,
Je humo elimuni? jaribu kuniambia,
Elimu nawambieni, kwamba haina kikomo.6. Kwiba nako kizoea, jela ni kwako nyumbani,
Maisha hukuzoea, si tabu ni kitu gani?
Hayo sijayakosea, kama si somo semeni,
Elimu nawambieni, kwamba haina kikomo.7. Hutakuwa na fitina, ukiwa safi rohoni,
Hutathaminika sana, uwapo wa kurubuni,
Nambieni la maana, siyo elimu jamani?
Elimu nawambieni, kwamba haina kikomo.8. Ujiweke ulevini, tabuni waogelea,
Magomvi bila kiini, yafaa nini ongea,
Na ukiwa ugenini, soni hutajionea?
Elimu nawambieni, kwamba haina kikomo.9. Niwapo ufukarani, mawazo hunifuata,
Wapi nitie mpini, cha tumboni kukipata,
Hapo nimo mafunzoni, uvivu nini waleta,
Elimu nawambieni, kwamba haina kikomo.10. Mambo mengi mumepata, kwa hiyo angalieni,
Jaribuni kuyafata, muyatie akilini,
La maana hukupata, usitie maanani,
Elimu nawambieni, kwamba haina kikomo.— D.P.B. Massamba
(a) Fafanua kwa hoja sita, mtazamo wa nafsineni kuhusu elimu kwa mujibu wa shairi hili. (alama 6)
(b) Bainisha vipengele vifuatavyo vya kimtindo katika ubeti wa tano: (i) tanakuzi; (alama 1) (ii) tashihisi. (alama 1)
(c) Eleza muundo wa shairi hili. (alama 4)
(d) Fafanua mbinu mbili ambazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi kutoka ubeti wa sita hadi wa kumi. (alama 4)
(e) Bainisha toni katika shairi hili. (alama 2)
(f) Andika ubeti wa kwanza katika lugha ya nathari. (alama 2)
Sehemu B: Riwaya
A. Matei: Chozi la Heri — Jibu swali la 2 au la 3.
2. "… alitaka kudakiza … lakini alijiasa. Hakukuwa na haja ya kuonyesha donda hili kwa viumbe ambao hawana imani."
(a) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
(b) Fafanua sifa sita za viumbe wanaorejelewa katika dondoo hili kwa mujibu wa muktadha huu. (alama 6)
(c) Kwa kurejelea hoja kumi kutoka kwenye riwaya hii, jadili madonda ya anayejiasa. (alama 10)
3. Jadili nafasi ya mwanamke katika kuendeleza ukiukaji wa haki za kibinadamu katika riwaya ya Chozi la Heri. (alama 20)
Sehemu C: Tamthilia
T.M. Arege: Bembea ya Maisha — Jibu swali la 4 au la 5.
4. (a) "… usitake sana kuhoji alacho kuku. Utachafukwa roho umchukie kuku bure. Wala usitake kujua nyuki ameitengenezea nini asali. Hutaila."
(i) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
(ii) Bainisha toni katika dondoo hili. (alama 2)
(iii) Tambua aina mbili za taswira katika dondoo hili. (alama 2)
(iv) Fafanua umuhimu wa anayeambiwa maneno haya katika kujenga tamthilia ya Bembea ya Maisha. (alama 6)
(b) Kudumu kwa asasi ya ndoa kunategemea juhudi za wahusika. Thibitisha kauli hii kwa kurejelea ndoa ya Yona na Sara katika tamthilia ya Bembea ya Maisha. (alama 6)
5. (a) Soma dondoo lifuatalo kisha ujibu maswali.
Sara: Mimi ninashukuru kwa hawa alionipa Mungu. Nikitaka zaidi nitakuwa mchache wa shukrani. (Kimya.) Dina, nimesemwa sana na kutukanwa kwa sababu ya hawa wasichana wangu. Wewe unajua yote yaliyosemwa, hadharani na faraghani. Si makanisani, si magengeni. Leo nikiviona vitoto hivi vilivyochekwa na kusimangwa jana, vikijiendeshea mambo yao, ninaridhika moyoni. Hata nikiitwa nitaondoka nikiwa nimeridhika. (Anatokwa machozi.)
(i) Changanua maudhui katika dondoo hili. (alama 3)
(ii) Bainisha toni katika dondoo hili. (alama 2)
(iii) Tambua mbinu tatu za lugha ambazo zimetumiwa katika dondoo hili. (alama 3)
(b) Jadili jinsi suala la utu linavyoshughulikiwa katika tamthilia ya Bembea ya Maisha. (alama 12)
Sehemu D: Hadithi Fupi
D.M. Lutomia na P. Muthama (Wah.): Mapambazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine — Jibu swali la 6 au la 7.
6. P.K. Kyovi: "Kila Mchezea Wembe"
(a) "… ni mtoto mdogo hapa alipo lakini ameneemekewa na mengi. Akili nyepesi masomoni yenye kunata mafunzo kuliko sumaku, urembo usiomithilika na ni mwenye kuuthamini utu wa mtu."
(i) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
(ii) Fafanua umuhimu wa mbinu mbili za kimtindo zilizotumiwa katika dondoo hili. (alama 4)
(iii) Eleza sifa nne za mrejelewa katika dondoo hili. (alama 4)
(b) Matumizi ya pombe yana athari hasi katika jamii. Thibitisha kauli hii kwa kurejelea hadithi "Kila Mchezea Wembe". (alama 8)
7. (a) Suala la umaskini limejitokeza katika hadithi "Pupa". Thibitisha. (alama 10)
(b) "Uwajibikaji katika jamii unachangia kuboresha maisha." Fafanua kauli hii kwa kurejelea hadithi "Ahadi ni Deni". (alama 10)
Sehemu E: Fasihi Simulizi
8. (a) Soma hadithi ifuatayo kisha ujibu maswali.
Hapo zamani za kale katika ujirani wa kijiji cha Tulia paliishi zimwi kubwa ajabu. Zimwi hilo lilikuwa la kutisha. Lilikuwa na jicho moja kipajini na jingine kisogoni. Amini usiamini, zimwi hilo pia lilikuwa na mikono mitatu na miguu minne. Laiti ungeliona! Zimwi hilo liliwahangaisha wanakijiji wa kijiji cha Tulia kila uchao. Wakati mwingine lilivamia na kubugia watu na mifugo wao. Zimwi liliendelea na tabia hii na kuwameza wanakijiji wote isipokuwa Doti. Hivi zimwi hili lilikuwa halishibi?
Doti alikuwa mfupi kama nyundo na mwembamba kama sindano. Pengine ndio maana zimwi halikudiriki kumtia kiganjani. Watu wote walipomezwa, Doti alijua kuwa wenzake wameshanyolewa na sharti atie chake maji. Alichonga kijiti kigumu chenye ncha kali.
Siku ya siku iliwadia. Zimwi lilinusa na kunasa harufu ya Doti kwa mba-a-a-li. Lilikwenda moja kwa moja hadi kijijini. Lilimtafuta Doti kila mahali. Doti alipoliona zimwi, alipiga moyo konde na kulikabili.
"Liwalo na liwe. Nitapigana nalo!" Doti alijisemea.
Doti alikuwa mwenye moyo wa simba. Alinyemelea chini ya tumbo la zimwi na kulidunga kwa kile kijiti alichokichonga. Tumbo la zimwi lilipasuka na wanakijiji wote pamoja na mifugo wao walitoka wakiwa hai. Doti alifurahi ghaya ya kufurahi. Wanakijiji walimwimbia nyimbo za kumsifu. Hadithi yangu imeishia hapa.
(i) Ainisha ngano hii kwa kuzingatia kipengele cha wahusika. (alama 2)
(ii) Fafanua mbinu nane za kimtindo ambazo fanani ametumia katika uwasilishaji wake. (alama 8)
(b) Wewe ni miongoni mwa wanaotambiwa ngano ya aina hii. Fafanua mambo sita ambayo wewe na wenzako mnaweza kuchangia ili kufanikisha uwasilishaji wa utambaji. (alama 6)
(c) Fafanua mikakati minne ambayo jamii inaweza kutumia ili kudumisha kipera hiki. (alama 4)