KCSE Revision AI kcserevision.app

KCSE 2021 Kiswahili Paper 3

The KCSE 2021 Kiswahili Paper 3 (102/3). Fasihi: riwaya, tamthilia, hadithi fupi, ushairi na fasihi simulizi. View it below, download it to print, or revise it with the AI tutor, which takes you through each question and marks your answers. Source: KNEC.

This file contains more than one paper for 2021; Paper 3 is inside.

102/3 · KISWAHILI · Karatasi ya 3 · FASIHI · Machi 2022 (KCSE 2021) · Muda: Saa 2½

Maagizo: Jibu maswali manne pekee. Swali la kwanza ni la lazima. Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani Riwaya, Hadithi Fupi, Ushairi na Fasihi Simulizi. Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.

Sehemu A: Tamthilia — P. Kea: Kigogo

1. Lazima
(a) "Akose? Asiya ni mwanamke halisi bwana! Amemweka Bi Husda hapa."
 (i) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
 (ii) Eleza vipengele viwili vya kimtindo alivyotumia msemaji kufanikisha uwasilishaji wa ujumbe. (alama 2)
 (iii) Fafanua sifa nne za anayeambiwa maneno haya. (alama 4)
(b) "Kuzorota kwa maadili kunachangia kuzorota kwa mahusiano ya kijamii." Thibitisha kauli hii kwa kurejelea tamthilia ya Kigogo. (alama 10)

Sehemu B: Riwaya — A. Matei: Chozi la Heri

Jibu swali la 2 au la 3.

2. Jadili nafasi ya mwanamke katika kuendeleza ukiukaji wa haki za kibinadamu katika riwaya ya Chozi la Heri. (alama 20)

3. (a) Changanua mtindo katika dondoo lifuatalo: (alama 10)

"Una bahati sana mwenzangu," alisema Kairu siku moja, "wewe hujapitia tuliyopitia. Tulitendwa ya kutendwa. Siku hiyo tulipofurushwa kwetu kama takataka tulitanga na njia bila kujua tuendako, mama mbele, sisi nyuma, mama amebeba kitindamimba ambaye baadaye alishindwa kukamilisha safari; roho yake changa ikakatika papo hapo mgongoni mwa mama, amemezwa na njaa na ugonjwa wa udhaifu wa mapafu. Mama alituelekeza kando ya njia, tukaingia kichakani kiasi. Sijui alikotoa kiserema alichokitumia kuchimba kaburi lenye kina cha haja, tukaufukia mwili wa ndugu yetu huku kilio cha uchungu na jitimai kikihanikiza kote."

(b) Jadili nafasi ya wahusika wafuatao katika kuijenga riwaya ya Chozi la Heri: (i) Cizarina; (alama 5) (ii) Tila. (alama 5)

Sehemu C: Hadithi Fupi — A. Chokocho na D. Kayanda (Wah.): Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine

Jibu swali la 4 au la 5.

4. A. Chokocho: Masharti ya Kisasa
"Alipokuwa kiguu na njia akimwinda kama kunguru … Ajabu lakini, kwa nini misumari ya nyuki inamwuma sasa ila si wakati ule wa tamaa ya ushindi ilipokuwa mbali …"
(a) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
(b) Bainisha toni katika kauli hii. (alama 2)
(c) Fafanua "misumari ya nyuki" kwa kurejelea hadithi Masharti ya Kisasa. (alama 14)

5. (a) "Suala la uozo wa kijamii limejitokeza katika hadithi Mame Bakari." Thibitisha. (alama 10)
(b) Jadili mchango wa wazazi katika maisha ya vijana kwa kurejelea hadithi Ndoto ya Mashaka. (alama 10)

Sehemu D: Ushairi

Jibu swali la 6 au la 7.

6. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

Mtu asiye heshima, aibu ya roho yake
Mfano wake tazama, kama popo mwendo wake
Wanaposhindwa wanyama, hudai ndege wenzake
Na ndege sio wenzake, wanaposhinda wanyama.

Na siku ya mapatano, ya ndege na wanyama
Yeye huwa ni miguno, halipati la kusema
Hana masikilizano, kwa ndege wala wanyama
Mtu kamaye daima, ni aibu kubwa mno.

Huwa hatamki neno, kama kinywa kimetuna
Hapati la mnong'ono, heshima hanayo tena
Hana heshima ya neno, wala heshima ya jina
Hapati kuonekana, hampi mtu mkono.

Hafai kuandamana, mtu huyo umwepuke
Kama alivyo hiana, juu ya nafsi yake
Na salama kwako hana, afadhali mtanuke
Hiana na roho yake, kwako hawi muungwana.

Mbaya mtu hiana, kuwa naye utajuta
Dunia ikikubana, na kusongwa na matata
Atakutupa mchana, mbinguni hakuna nyota;
Ni mambo yanatukuta, na kisha hutendekana.

(S. Robert)

(a) Eleza ujumbe wa shairi hili. (alama 4)
(b) Bainisha nafsineni ya shairi hili. (alama 2)
(c) Fafanua umuhimu wa uhuru wa kishairi uliotumiwa katika shairi hili. (alama 6)
(d) Eleza dhima ya aina mbili za urudiaji zinazojitokeza katika shairi hili. (alama 4)
(e) Bainisha tamathali za usemi katika ubeti wa kwanza na wa pili. (alama 2)
(f) Andika ubeti wa mwisho kwa lugha ya nathari. (alama 2)

7. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

Nalilia mazingira yetu haya
Hakuna kilicho safi
Vyote ni kombo
Mrama vimekwenda.

Tazama mto huu
Mto utambao katikati mwa jiji kuu
Jiji la uzungu na usasa
Lenye warembo na wakwasi
Wanaolivuka bila fahamu
Wanaolilima bila kujali
Wanalifumbia macho ilhali lipo!

Najua mwakani watakuja usafi kulitia
Usafi ndugu wa siku moja
Eti kuupa mji sura!
Wanaukosha mji, si mto!

Ni mto ulioona mengi na makubwa kushuhudia
Lakini kwa kimya ndugu zangu unakwenda
Labda kwa uchovu na bughudha
Ningekuwa mimi ningepaaza sauti:
"Punguzeni bughudha. Msinitwike mizigo yenu
Maana mimi mnanibebesha mizigo yenu
Na minyororo ya uchafu kunitia
Kusudi mpate safika. Tangu lini
Mto kukoshwa kwa sabuni? Hamjui
Mto husafisha dhambi?"

Lakini nionavyo ndugu
Taswira ya mto huu
Ni taswira kamilifu ya kizazi chetu!
Kizazi baina ya kilichopita na kijacho.

(Limenukuliwa kutoka: Tumu ya Ushairi*)*

(a) Eleza ujumbe wa shairi hili. (alama 5)
(b) Onyesha mbinu mbili za uhuru wa kishairi katika shairi hili. (alama 2)
(c) Bainisha vipengele vifuatavyo vya kimtindo katika shairi hili: (i) tashihisi; (ii) swali la balagha; (iii) kinaya. (alama 3)
(d) Onyesha aina mbili za urudiaji zinazojitokeza katika ubeti wa pili. (alama 2)
(e) Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 1)
(f) Fafanua aina tatu za taswira kwa kurejelea shairi hili. (alama 3)
(g) Eleza toni ya shairi hili. (alama 2)
(h) Andika ubeti wa tatu katika lugha ya nathari. (alama 2)

Sehemu E: Fasihi Simulizi

8. Soma hadithi ifuatayo kisha ujibu maswali.

Hapo zamani za kale Nungunungu na Fisi walikuwa marafiki wa kufa kuzikana. Walizilea familia zao pamoja. Nungunungu aliwafaa watoto wa Fisi kwa nafaka naye Fisi aliwafaa wa Nungunungu kwa nyama. Wanyama wengi waliuhusudu urafiki wao. Hata hivyo, Sungura hakusita kumtahadharisha Nungunungu mara kwa mara.

"Ndugu," Sungura alisema siku moja, "Sijui kilichokuvuta kwa huyu mwenzako, ila nataka ujue kwamba mla mizoga haaminiki, haitakuwa ibra watoto wako wakigeuzwa kitoweo chake."

Nungunungu aliyatia maneno ya Sungura kwenye mizani, akataka kuyaamini, lakini moyo wake ukamuasa dhidi ya haya. Unajua tena mjukuu wangu kauli za mwenye hila hazisadikiki kwa urahisi. Nungunungu alijisemea moyoni, "Simtarajii ndugu yangu huyu aniendee kinyume. Nimeishi naye kwa miaka mingi, nikimfaa kwa jua naye akinifaa kwa mvua, tukizungumza ya kupwa na kujaa, tukilizana kwa furaha na simanzi. Itatokeaje anisaliti baada ya muda wote huu? Na iwe hiyo tamaa wamsingiziayo lakini kuwafanya kitoweo watoto wangu mimi ambaye hujisabilia kuwalea watoto wake mwenyewe anapomezwa na msitu akitafuta mizoga! Haiwezekani. La! Hasha!"

Basi mjukuu wangu Nungunungu aliyatia masikio nta; akapuuzilia mbali ushauri wa jirani yake Sungura. Hakuona haja ya kuufuata ushauri huu kwani alijua kwamba ikiwa kweli Fisi alikuwa na doa, ukweli ungemdondokea viganjani mwake.

Mbivu na mbichi ilibainika wakati kiangazi kikubwa kilikumba kijiji walikoishi Nungunungu na Fisi. Ukame ulibisha hodi. Njaa na ukosefu wa maji ukatishia kukipukutisha kizazi kizima cha wanyama.

Hata hivyo, Nungunungu hakuwa na wasiwasi. Unaweza kusema kwamba yeye alikuwa kondoo mwenye manyoya tele. Maghala yake yalishiba yakatapika nafaka. Hivyo mng'ato wa ukame haukumwathiri.

Kiangazi kilizidi kung'ata naye Nungunungu akaanza kuona muujiza wa kupungua kwa nafaka ghalani siku baada ya siku. Alipomuuliza Fisi, Fisi alikuja juu. "Nani mwingine ila yule goigoi, Sungura? Mimi kila mara hujituma kuitafuta mizoga, japo mizoga yenyewe imeadimika. Wakati mwingine hulazimika kujiulia mwenyewe."

Sungura aliposikia hayo alijinyamazia tu. Alijua kwamba za mwizi ni arobaini. Alimwambia Nungunungu, "Umdhaniaye ndiye siye." Kisha akaondoka. Jioni hiyo Sungura alitia gundi kwenye lango la ghala la Nungunungu na kujiendea zake kulala.

Alfajiri mbichi Nungunungu aliamshwa na sauti ya kite. Alipotoka nje alimpata Fisi kaning'inia ghalani hivi, likawa lile la "Mwenye macho haambiwi tazama." Mjukuu wangu, ingekuwa wewe ungemfanyia nini rafiki yako huyu wa dhati?

Hadithi yangu inaishia hapo. Naomba mbuzi wangu wale majani mabichi na wako wafe kwa kiangazi.

(a) (i) Ainisha ngano hii kwa kurejelea kigezo cha wahusika. (alama 2) (ii) Fafanua mbinu sita ambazo mtambaji ametumia kufanikisha uwasilishaji wa ngano hii. (alama 6) (iii) Eleza shughuli tatu za kiuchumi ambazo zimejitokeza katika utungo huu. (alama 3) (iv) Eleza majukumu manne ya fomyula ya kumalizia katika utungo huu. (alama 4)
(b) Kipera cha ngano kinaendelea kufifia katika jamii yako. Pendekeza mbinu tano ambazo jamii yako inaweza kutumia kukinga dhidi ya hali hii. (alama 5)

More Kiswahili papers